Halloween party ideas 2015
Showing posts with label SIASA NA JAMII. Show all posts

HATIMAYE, Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad ametoa msimamo wake na chama chake kufuatia mazungumzo ya siri ya kutafuta suluhu ya mkwamo wa kisiasa unaotokana na tangazo la kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar.

Akizungumza leo na waandishi wa habari katika hotel ya kitalii ya Serena jijini Dar es Salaam, Maalim Seif amesisitiza kuwa hoja ya kurudia uchaguzi wa Zanzibar kama inavyoelezwa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), haina msingi, haikubaliki na sio halali kikatiba.

“Hoja ya kurudia uchaguzi haina msingi, haina uhalali, ni hoja ambayo inaweza kuzaa fujo na vurugu na inaweza kuleta mzozo mkubwa wa kikatiba wa kisheria. Sidhani kama tunataka kuwapeleka huko watanzania,” alisema Maalim Seif.

Makamu huyo wa kwanza wa rais wa Zanzibar ameeleza kuwa tayari wameshafanya vikao nane vilivyowashirikisha wagombea urais pamoja na marais wastaafu wa Zanzibar lakini hawakukubaliana kurudia  uchaguzi kama baadhi ya viongozi wa CCM walivyoeleza.

Aidha, Maalim Seif amekanusha kilichoelezwa na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd baada ya kukutana na Rais John Magufuli, kuwa rais alisema warudie Zanzibar kujiandaa na marudio ya uchaguzi kwani rais hakusema hivyo alipokutana naye.

Maalim Seif amesema kuwa ana imani kubwa na rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli katika kuleta maridhiano na ufumbuzi wa mgogoro wa Zanzibar kutokana na mazungumzo aliyofanya naye hivi karibuni katika Ikulu ya Magogoni jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa endapo uchaguzi mkuu utatakiwa kurudiwa, zipo changamoto nyingi za kikatiba ambazo zitakwamisha zoezi hilo hivyo uchaguzi huo hautawezekana.

Ametaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na kupitishwa kwa fedha za kugharamia uchaguzi na baraza la wawakilishi ambalo hivi sasa halipo kwa kuwa limefikia ukomo wake.

Mbali na hilo, Maalim Seif alieleza kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salum Jecha anapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria na kinidhamu kwa kutoa tamko lisilo halali la kufuta uchaguzi huo huku akifahamu dhahiri kuwa hana nguvu hiyo kikatiba.

Ameitaka ZEC iongozwe na makamu mwenyekiti wake kwa mujibu wa katiba pamoja na wajumbe wengine kukamilisha utaratibu wa kuhakiki matokeo ya uchaguzi na kumtangaza mshindi.

Maalim Seif ameeleza kuwa anafahamu dhahiri kuwa kuna mpango wa kutangaza kwa nguvu marudio ya uchaguzi Februari 28 mwaka huu, lakini yeye pamoja na chama chake hawatakubali.


Muda mfupi baada ya Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad kutangaza kasoro na athari za kurudia Uchaguzi uliofutwa kinyume cha sheria na Jecha Salim Jecha, viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wametangaza kuwa uchaguzi  huo lazima urudiwe.

Wakizungumza jana na vijana wa chama cha Mapinduzi katika viwanja vya Maisara waliokuwa wamekusanyika kwa ajili ya matembezi ya kuunga mkono Mapinduzi ya Zanzibar,viongozi wa juu wa chama hicho walisisitiza kuwa uchaguzi wa Zanzibar upo pale pale na utarudiwa kadiri tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) itakavyotangaza.

Wa kwanza kutoa msimamo huo alikuwa ni Makamu wa pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, aliyesema kuwa uchaguzi huo utarudiwa hata ikiwezekana vyama vyote vikijitoa CCM kitashiriki peke yake

“Uchaguzi wa marudio upo pale pale, tunajua uchaguzi ulifutwa kihalali, mjitayarishe kwa uchaguzi wa marudio. CUF wamesema watatumia nguvu ya umma, tunawakaribisha na wataona matokeo yake” alisema Balozi Iddi.

Katika mkutano huo uliokuwa unarushwa moja kwa moja na kituo cha Televisheni cha ZBC, Dk  Alli Mohamed Shein alipongeza msimamo wa Balozi Iddi, na kusema atabaki kuwa rais hadi uchaguzi utakaporudiwa.

Dk Shein alisema yupo madarakani kwa kushauriwa na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar kwamba hajavunja katiba na kama itatokea mahakama ikatoa ufafanuzi kuwa anakosea kuwepo hapo kikatiba basi ataondoka madarakani

“Mahakama ikisema nakosea nitaondoka, Rais yupo Baraza la Mapinduzi lipo na Mawaziri wapo, nitaita waandishi wa habari Ikulu na mimi nimjibu Maalim Seif kwani kuna mengi amenisingizia” alisema

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, DCP Simon Sirro.

Stori: Na Makongoro Oging’, UWAZI
DAR ES SALAAM: Baadhi ya benki nchini zinadaiwa kuajiri baadhi ya wafanyakazi walio kwenye mtandao wa majambazi kutokana na wateja wengi kupigwa risasi na kufa wakitoka kuchukua pesa, uchunguzi wa baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi Tanzania umebaini.
Hayo yalisemwa na baadhi ya askari hao wiki iliyopita walipozungumza na mwandishi wetu na kusema kwamba, waajiri wasipokuwa makini katika kuajiri watashangaa kuona wateja wao wanapigwa risasi na kuuawa kila kukicha.

“Haiwezekani kuwa wanaonyang’anywa fedha ni wale wanaotoka kuchukua benki kuliko wanaopeleka! Ina maana wezi wapo katika baadhi ya mabenki hivyo kunatakiwa kuwepo na umakini wakati wa kuwaajiri,” alisema askari mmoja kutoka makao makuu ya jeshi hilo, Dar akiomba hifadhi ya jina lake kwa vile yeye si msemaji.
Afande huyo aliendelea kusema kuwa, baadhi ya wafanyakazi wasio waaminifu wa benki hizo wanapoona mteja anachukua fedha nyingi hufanya mawasiliano kwa njia ya simu kuwaeleza majambazi walio nje namna alivyovaa mteja huyo na kiasi cha fedha alichochukua.
Uchunguzi zaidi unaonesha kuwa, endapo hali hiyo haitadhibitiwa haraka huenda wananchi wakapatwa na hofu ya kuweka fedha zao benki kwa kuogopa kuporwa na kupigwa risasi wakienda kuzichukua.

Uwazi mwishoni mwa wiki iliyopita, lilimtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, DCP Simon Sirro (pichani) ambapo alikiri kuwepo kwa baadhi ya wafanyakazi wenye mtandao na majambazi huku akisema jeshi lake limeweka mikakati kuhakikisha mtandao huo unasambaratishwa mara moja.

“Ni kweli kwamba, baadhi ya mabenki, si yote, yameajiri baadhi ya wafanyakazi, si wote wenye mtandao na majambazi. Kwa hiyo hata wao ni majambazi tu.
“Sasa tumejipanga vizuri ikiwa ni pamoja na kukamata pikipiki zinazohusika katika uhalifu. Pia tumeamua kuweka makachero nje na ndani ya mabenki, wapo polisi wa miguu, pikip iki na magari. Nina uhakika tutawadhibiti,” alisema Kamanda Sirro.
Aliendelea kusema kuwa, majambazi waliopo katika Kanda ya Dar es Salaam waanze kufunga virago kwani bila kufanya hivyo wajue watakamatwa wote na mtandao wao kumalizika. Pia aliwataka wamiliki wa mabenki kuwa makini wakati wa kuajiri wafanyakazi ili kuwapata wenye sifa njema na kuweka imani kwa wateja wao.

Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishina Suleiman Kova aliwahi kutamka kuwa, baadhi ya wafanyakazi wa ndani wa baadhi ya benki wana ushirikiano na majambazi. Akawatahadharisha wamiliki kuwa makini wakati wa kuajiri.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Yustino Ndugai.

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU UTEUZI WA WABUNGE KWENYE KAMATI ZA KUDUMU ZA BUNGE.
Katibu wa Bunge anatoa taarifa kwa umma kwamba:
(a) Kwa mujibu wa Kanuni ya 116 (3) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Aprili, 2013, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano amepewa mamlaka ya kuteua Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge kwa namna ambayo itawezesha kila Mbunge kuwekwa kwenye Kamati mojawapo. Katika kufanya uteuzi huo, Spika huzingatia vigezo mbalimbali vilivyoainishwa katika Kanuni ya 116 (5);(b) Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Mhe. Job Yustino Ndugai (MB), ametekeleza mamlaka yake ya uteuzi kwa mujibu wa Kanuni tajwa hapo juu, kwa kuwateua kwanza Wabunge Kumi na Tano (15) kuwa Wajumbe wa Kamati ya Kanuni za Bunge.
Kamati hiyo imeundwa na kutangazwa kabla ya Kamati zingine ili ifanye marekebisho ya Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge kuhusu majukumu ya Kamati zingine za Bunge kwa kuyashabihisha na majukumu ya Serikali kwa kuzingatia Muundo wa Baraza la Mawaziri lililopo sasa.
Lengo kuu ni kuleta urahisi, ufanisi na tija kwa Bunge katika kuisimamia na kuishauri Serikali;
(c) Kwa msingi huo, Kamati ya Kanuni za Kudumu za Bunge, ambayo Spika ndiye Mwenyekiti wake na Naibu Spika ni Makamu Mwenyekiti, Kiongozi wa Upinzani na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambao ni Wajumbe kwa nyadhifa zao itakutana katika Ofisi ya Bunge, Dar es Salaam siku ya Ijumaa tarehe 15 Januari, 2016 saa tano kamili asubuhi katika Ukumbi wa Spika. Wajumbe wengine ni: –
(i) Mhe. Makame Kassim Makame, MB. – Jimbo la Mwera;
(ii) Mhe. Tundu Antipas Mughwai Lissu, MB. – Jimbo la Singida Mashariki;
(iii) Mhe. Jasson Samson Rweikiza, MB. – Jimbo la Bukoba Vijijini;
(iv) Mhe. Ally Saleh Ally, MB. – Jimbo la Malindi;
(v) Mhe. Magdalena Hamis Sakaya, MB. – Jimbo la Kaliua;
(vi) Mhe. Salome Wycliff Makamba, MB. – Viti Maalum;
(vii) Mhe. Dkt. Jasmine Tiisekwa Bunga, MB. – Viti Maalum;
(viii) Mhe. Zainab Athman Katimba, MB. – Viti Maalum;
(ix) Mhe. Balozi Adadi Mohamed Rajab, MB. – Jimbo la Muheza;
(x)Mhe. Dkt. Charles John Tizeba, MB. – Jimbo la Buchosa; na
(xi) Mhe. Kangi Alphaxard Lugola, MB. – Jimbo la Mwibara.
(d) Spika atakamilisha uteuzi wa Wajumbe katika Kamati zingine za Bunge kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Pili wa Bunge tarehe 26 Januari, 2016, Mjini Dodoma ili kutoa fursa kwa Kamati zote kuchagua Viongozi wake na kuandaa Mpango Kazi kwa mwaka 2016/17; na
(e) Wabunge wote wanatangaziwa kuwa wawe wamefika Dodoma tarehe 20 Januari, 2016 tayari kwa kuanza kwa Kamati za Bunge na Mkutano wa Bunge, isipokuwa Kamati ya Wabunge (Caucus) wote wa Chama cha Mapinduzi wanatakiwa kuwa Mjini Dodoma tarehe 17 Januari, 2016 kwa Mkutano wao.
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano,
Ofisi ya Bunge,
S. L. P. 9133,
DAR ES SALAAM.
11 Januari, 2016.


Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir kwa mara ya kwanza amewaomba radhi raia wa nchi hiyo kutokana na mateso na dhiki ambayo wamepitia wakati wa mzozo wa kisiasa uliodumu miaka miwili.
Bw Kiir amesema kuomba msamaha ndiyo hatua ya kwanza katika kufanikisha maridhiano nchini humo.
Amechukua hatua hiyo wakati wa kufungua rasmi mkutano mkuu wa chama tawala cha SPLM.
Kutoelewana katika mkutano sawa mwaka 2013 kulitangulia jariibo la mapinduzi ya serikali nchini humo na mapigano yaliyodumu miezi mingi.
Mkataba wa Amani ulitiwa saini mwezi Agosti mwaka jana mjini Addis Ababa, ingawa Rais Kiir alitia saini mkataba huo shingo upande.
Jana, pande zilizohusika katika mzozo huo ziliafikiana kuhusu kugawana nyadhifa za uwaziri katika baraza la mawaziri la serikali ya umoja.
“Hebu niwaambie, wenzangu, kwamba mimi, kama Mkristo, imenibidi kujitafakari jambo ambalo ni hatua kuu kwetu sote kama taifa moja na kufikia uwiano na umoja,” alisema Bw Kiir.

Mshukiwa wa ugaidi aliyeshtakiwa kuwaingiza watoto katika kundi la al-Shabab amehukumiwa kufungwa jela miaka 20 na mahakama Mombasa.

Samuel Wanjala Wabwire almaarufu Salim Mohammed alishtakiwa kuwapa watoto mafundisho ya itikadi kali.
Alikuwa ameshtakiwa pia kuwa mwanachama wa kundi hilo kutoka Somalia.

Watoto waliotoa ushuhuda kwenye kesi yake wanasema aliwafunza kwamba Wakristo ni makafiri ambao wanafaa kuuawa.
Baadhi ya watoto hao walisilimu.
Bw Wabwire alikuwa mwalimu wa shule ya msingi na pia imam katika Masjid Jihad.

Alikabiliwa pia na shtaka la tatu la kueneza itikadi kali na vita vya kidini. Anadaiwa kutoa mafunzo ya karate msikitini.
Alikamatwa mwezi Juni mwaka 2015 eneo la Kaloleni, jimbo la Kilifi.


Tanzania imeanza rasmi operesheni ya kuwasaka na kuwafurusha raia wa kigeni wanaoishi na kufanya kazi nchini humo kinyume cha sheria.

Naibu waziri wa mambo ya ndani wa Tanzania Hamad Masauni ameambia wanahabari kwamba operesheni hiyo imeanzishwa baada ya kubainika kwamba kuna raia wengi wa kigeni wanaofanya kazi Tanzania kinyume cha sheria.

Operesheni hiyo hiyo inafanyika siku chache baada ya wizara inayohusika na ajira kumuagiza kamishna wa kazi nchini humo kufuta vibali vya kazi vya muda kwa wageni.

"Serikali haiwezi kukaa kimya wakati vijana wanakosa ajira huku kazi zile walizotakiwa kufanya zikifanywa na raia wa kigeni,” Bw Masauni amenukuliwa na gazeti la Mwananchi.
Afisa wa uhamiaji wa mkoa wa Dar es Salaam John Msumile amesema wanatarajia kuwakamata wageni zaidi ya 350.

Kuhusu vibali va kazi vya muda, Bw Masauni amesema serikali itaandaa utaratibu mwingine wa kushughulikia watu wanaotaka kufanya kazi Tanzania kwa muda.

Hii ni baada ya serikali kupokea malalamiko mengi kuhusu suala hilo.
Mwishoni mwa mwaka waziri katika afisi ya waziri mkuu anayehusika na ajira Jenista Mhagama pamoja na naibu waziri Anthony Mavunde walifanya ziara za kushtukiza katika kampuni mbalimbali.

Waligundua raia kadha wa kigeni waliokuwa wakifanya kazi bila vibali halali.


Somalia imetangaza kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Iran ikiituhumu kwa kuingilia masuala ya ndani ya Somalia.

Serikali ya Somalia imewapa maafisa wote wa ubalozi wa Iran mjini Mogadishu muda wa saa 72 (siku tatu) wawe wameondoka nchini humo.
Uamuzi huo umechukuliwa baada ya mkutano wa baraza la mawaziri wa Somalia.

“Hatua hii imechukuliwa baada ya kutathminiwa kwa kina na kutokana na hatua ya Jamhuri ya Iran kuendelea kuingilia masuala ya ndani ya Somalia,” taarifa kutoka wizara ya mashauri ya kigeni ya Somalia imesema.

"Jamhuri ya Somalia inaitaka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuheshimu uhuru wa mataifa yote kwa mujibu wa sheria za kimataifa, Mkataba wa Vienna kuhusu Uhusiano wa Kidiplomasia wa mwaka 1961 na tamaduni za uhusiano wa kidiplomasia.
Powered by Blogger.

Powered by themekiller.com